Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kuwa Serikali itayafuta makampuni ya ulinzi binafsi nchini ambayo yanaajiri askari vikongwe pamoja na wasiokuwa na mafunzo ya askari wa akiba (mgambo) wala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Amesema kuwa Wizara yake haiwezi kucheza na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi kwa kuyaacha makampuni hayo yaendelea kuajiri vikongwe ambao hawezi kushika silaha za moto na pia mara kwa mara huwa wanasinzia kiasi kwamba muda wowote wanaweza wakanyang’anywa silaha na majambazi ambao wanazitafuta silaha kwa ajili ya kufanyia uhalifu.

Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Kata ya Nansimo, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda Mkoani Mara, ambapo amesema kuwa kutokana na upungufu wa askari, Serikali iliruhusu kuwepo na makampuni binafsi ya ulinzi kwa ajili ya kusaidia masuala ya ulinzi na usalama nchini.

Aidha, amesema kuwa miaka ya hivi karibuni Serikali imeendelea kuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba kwa wale wanaopita katika Jeshi la Akiba ambao wanaitwa Mgambo, na wale wanaopitia katika Jeshi la Kujenga Taifa, maeneo hayo mawili yasaidie kuzalisha askari ambao watachukuliwa na Makampani ya Ulinzi ili waweze kufanya kazi kwasababu wanauzoefu wamefundishika, wanajua jinsi ya kubeba na kutumia silaha za moto.

“Lakini niendelee kusikitika, baadhi ya makampuni, tumeshuhudia yanaendelea kuajiri askari ambao wamechoka, askari ambao wamestaafu kwa mujibu wa umri wao, kwa maana hawawezi kufanya kazi tena hizi za kiaskari, lakini wanaajiriwa tena katika makampuni haya ya ulinzi,’ amesema Lugola

Waziri Lugola amesema kuwa kutokana na changamoto hiyo, Serikali inakaribia kukamilisha kuwepo na sheria ya makampuni hayo ya ulinzi, ambayo itasimamia vizuri makampuni yote nchini, na sheria hiyo itaenda kudhibiti pia masuala ya ajira kwa askari hao.

“Unaona mzee anatoka kazini asubuhi na bunduki yake kachoka hatua ishirini tu ameona mti pale kuna kivuli anafika hapo anaanza kusinzia mzee wa watu na bunduki, hata unifomu zenyewe hazimkai vizuri, kachokaa, eti huyo ni askari wa kampuni binafsi ya ulinzi, haiwezekani, silaha hizi zinahitaji umakini katika kubeba na katika kutumia, na wahalifu nao wanazitafuta silaha za namna hii, wakigundua mahala fulani kuna walioajiriwa ni wachofu, wapo hoi taabani hao ndio wanaonyang’anywa bunduki,” ameongeza Lugola.

Hata hivyo, amelielekeza Jeshi la Polisi, wahakikishe kuwa Makampuni hayo yanaajiri askari ambao wanasifa za kufanya kazi hiyo, pamoja na wahakikishe wanaajiri askari wenye sifa na kuwalipa askari hao vizuri, kwa kuwa baadhi ya wamiliki wa kampuni hizo wamekua wakiwatapeli, kutokuwalipa, na wengine wanakopwa na ofisi zao.

 

Marekani yatamba kutungua ndege ya kivita ya Iran
Kim Kardashian atinga Ikulu ya Marekani kumtetea Rapa Asap Rocky