Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama ameshauri uongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu (Makamu Saccos) kuwa na ubunifu katika utendaji ili kuleta manufaa zaidi kwa wanachama wake.

Mhagama ameyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama wa Chama hicho uliofanyika Januari 19, 2017 mkoani Dodoma.

Katika Mkutano huo Mhagama amesisitiza kuwepo na mikakati madhubuti ya kubuni miradi itakayowawezesha chama kuwa na vyanzo vyake vya mapato na kuwa na mikakati ya kuongeza wanachama wapya kwa kuzingatia umuhimu wa chama hicho.

“Ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kubuni miradi, kuongeza wanachama pamoja na kuwa na vitu vya kiupekee na vya kiufanisi vitakavyokisaidia chama kuwa imara katika utendaji wake”, amesema Waziri Mhagama.

Hata hivyo, amesema kuwa chama hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake amabapo wengi wao wamekuwa na maendeleo mbalimbali kutokana na uwepo wa fursa za mikopo isiyokuwa na masharti magumu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Joseph Muhamba ameahidi kuyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa na Waziri na kuyaweka katika vitendo ili kuhakikisha chama kinaongeza mbinu za ubunifu ikiwemo eneo la kuongeza wanachama wapya na kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wanachama waliopo.

 

 

Hapi: Dar hakuna njaa,tuna chakula cha kutosha
DC Iringa aagiza msako kwa waliofaulu na kutokwenda shuleni