Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Leo amezindua Mradi wa Usambazaji wa Maji Kutoka Kisarawe-Pugu-Gongolamboto na maeneo ya jirani Wenye thamani ya shilingi bilioni 6.9 ambapo amewapongeza DAWASA kwa jitihada kubwa wanazofanya kusogeza huduma ya maji kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Shule ya Sekondari Pugu, Samia amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya maji na kulipa bili za maji kwa wakati.
Aidha, Samia amesema kama DAWASA itaendelea na kasi hiyo ana matumaini makubwa kuwa ifikapo mwaka 2025 kilio cha uhaba wa maji Dar es salaam kitabaki kuwa historia ambapo kwa mujibu wa DAWASA hadi kufikia sasa upatikanaji wa maji jijini humo mefikia asilimia 92.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge amesema Mkoa huo umejipanga vizuri kuhakikisha unasimamia kikamilifu miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Serikali jijini humo, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Aidha, Kunenge ameipongeza DAWASA kwa kuweza kujiendesha, jambo linalopelekea miradi mingi kwa sasa kutekelezwa kwa fedha za ndani na kuonyesha jinsi ambavyo Mamlaka hiyo imedhamiria kufanya mageuzi kwenye suala la upatikanaji wa maji safi na salama.
Naye Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema tangu Serikali ya awamu ya Tano iingie Madarakani wamefanikiwa kutekeleza miradi ya maji Dar es salaam yenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni moja.
Hata hivyo, amesema mradi huo wa Pugu itawezesha kufikisha huduma ya Maji kwa wakazi wa Gongolamboto, Chanika, Zingiziwa, Banana, Ukonga, Segerea na maeneo yote ya jirani.