Burkina Faso tayari imeripoti kisa cha mtu mmoja kufariki dunia kufuatia virusi vya Corona ambavyo kwa sasa vimekuwa ni janga la dunia nzima kufuatia visa kadhaa kuripotiwa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Ambapo aliyekuwa makamu wa rais wa pili wa Bunge la Taifa hilo amefariki dunia siku ya Jumanne ya Machi 17, 2020 huku kisa kikitajwa kuwa ni kirusi cha Corona.
Marie-Rose Compaoré, alikuwa mwenye umri wa miaka 62, mbali na kuugua ugonjwa wa Corona alikuwa anaugua ugonjwa wa kisukari.
Prof. Martial Ouedraogo ambaye ndiye anasimamia visa vya Covid-19 nchini humo amesema kuwa kifo cha kiongozi huyo kimewashtua sana na kimewafanya kuwa makini katika kila hatua wanayochukua kupambana dhidi ya kirusi hiki cha Corona kwani ni hatari sana kwa nchi na dunia kiujumla.
“Tukio hili la kuhuzunisha linatushinikiza kila mmoja kutambua athari ya janga hili mbele yetu,” alisema profesa huyo.
Burkina Faso imeripoti visa 20 vya wagonjwa wa corona hadi sasa.
Aidha, kisa cha kifo kilichosababishwa na virusi vya Corona kilitangazwa pia Sudan Machi 13, 2020 ambapo mwanamume mmoja mwenye miaka 52 ambaye alikuwa amesafiri kutoka Taifa la Milki za Uarabuni (UAE) alielemewa na ugonjwa huo na kufariki dunia.