Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameongezewa muda wakukaa karantini siku saba, baada ya kumaliza siku 14 za awali aliporejea nchini kutoka Cuba ambako kuna waathirika wa Corona 260 na vifo sita.
Juzi balozi Iddi alituma video iliyorekodiwa, akieleza kuwa yeye na timu yake wameshakaa katika karantini kwa siku 14 kama taratibu za serikali zinzvyoelekeza.
Pamoja na kugundulika kuwa hana maambukizi, balozi Iddi amesema ameshauriwa na wataalamu wa afya kuongeza siku nyingine saba za karantini.
Waziri wa afya wa Zanzibar amesema suala la watu kuwekwa karantini halichagui mtu, ” haliangalii kiongozi wa serikali au mtu binafsi kwa kuwa kila anayetoka nje ya nchi anatakiwa kukaa katika karantini kwa siku 14 na kupimwa afya yake kama ana virusi vya corona”.
Aidha balozi Iddi ametoa wito kwa watu kuwa wanapaswa kuchukulia suala la kukaa Karantini ni tahadhari yenye dhamira njema ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Covid – 19.
Ikumbukwe kuwa Tanzania imetangaza watu waliopata maambukizi ya corona 20, huku mmoja akipoteza maisha na wengine watatu wakipona, na waliobaki hakuna aliye katika hali mbaya.