Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza wanunuzi waliochukua tumbaku za wakulima bila kuwalipa fedha zao, wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Majaliwa, ametoa agizo hilo Septemba 9, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika, AMCOS na wakulima wa tumbaku kutoka wilaya za Urambo na Kaliua, mkoani Tabora.
Amesema, “Tumbaku katika mkoa wa Tabora ni uchumi, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya wizara, mkoa, wilaya, kata na hata vijiji simamieni ushirika kwenye maeneo yenu, ushirika ni uchumi, sote tuwajibike kwa pamoja, tuhakikishe ushirika unapata mafanikio.”
Majaliwa ameongeza kuwa, Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayebainika kuhujumu ushirika nchini kwani imedhamiria kuuboresha na inataka Mkulima anufaike na jasho lake.
Waziri Mkuu, pia amewaagiza viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kushirikiana na Wakulima kutatua matatizo yao na kuwataka viongozi wa Serikali kusimamia mwenendo wa ushirika na kuhakikishe hakuna migogoro, wizi wala dhuluma.
“Kutaneni na viongozi wa mkoa na wilaya na muwaeleze changamoto zenu, viongozi wa Serikali nanyi wapokeeni na muwasikilizena hatua zichukuliwe kwa watakaowadhulumu wakulima.”
Aidha ameongeza kuwa, kitendo cha viongozi wa AMCOS kwenda kwa Waziri Mkuu na kuwasilisha kero zao wakati katika maeneo yao wapo watatuzi wa shida zaokinaonesha lipo tatizo na kuwasisitiza viongozi wa halmashauri kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa ushirika nchini wakamilishe agizo lake alilolitoa mwaka jana, la kuandaa kanzidata ya wakulima ili kuiwezesha Serikali kuwatambua wakulima na kurahisisha utoaji huduma.