Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi, Anne Makinda amesema zoezi zima la Sensa litakalofanyika Agosti 23, 2022 si la siku moja na litafanyika kwa siku sita na kwamba makarani wote watakuwa na vitambulisho Maalumu na kabla ya zoezi hilo viongozi wa mitaa na vijiji watapita katika kila kaya kuwatambulisha makaranı hao.
Makinda amesema hayo akizungumza katika kipindi maaalum na Dar24 media kuhusu zoezi zima la Sensa na maandalizi yake na hatua zilizofikiwa mpaka hivi sasa.
“Hakuna mtu atakaekuja bila kutambulishwa na kiongozi wa Mtaa, Karani wa Sensa lazima awe na kitambulisho, na awe ametambulishwa na Kiongozi wako wa eneo unaloishi,” amesema Makinda.
Amesema zoezi zima la Sensa linaweza kufanyika kwa siku kadhaa kwa sababu makarani wa Sensa hawawezi kukamilisha kwa siku moja ambayo imepangwa na serikali hivyo Watu waendelee na shughuli zao ila wahakikishe wanaweka rekodi ya watu waliolala usiku wa kuamkia Agosti 23, kwenye kaya zao.
“Sensa imepangwa ni tarehe 23 Agosti, lakini zoezi hili linaweza kwenda kwa siku kadhaa mbele kwa sababu makarani wataenda kaya kwa kaya na hawatamaliza kwa siku moja na haitakuwa siku ya mapumziko, wataanza Saa 6 na dakika 1 usiku. Tunaomba watu wote waweke rekodi ya waliolala katika nyumba yako usiku wa kuamkia tarehe 23 ili Karani atakapopita apate idadi kamili,” Anne Makinda, Kamisaa wa Sensa.
“Maswali katika zoezi la Sensa ni ya kawaida kabisa, kama Umri wako, idadi ya wanafamilia, shughuli zako, elimu ya watoto ndani ya kaya yako, kama kuna walemavu nk. Pia katika Dodoso la Jamii atakayehojiwa ni Kiongozi kama kuna Shule ngapi? huduma za maji, Mitandao ya simu, barabara,” amesema.
Makinda ameongeza kuwa kuna watu watatakiwa kuhojiwa kabla ya usiku wa Agosti 23 kwa sababu tofauti ikiwemo wasafiri wa mabasi ambapo watapewa vitambulisho ili kuwatambua wasirudie kuhesabiwa.
“Watakaohojiwa kabla ya tarehe 23 mfano wasafiri wa ndege, mabasi, hao watapewa vitambulisho maalumu ambavyo vitawatambulisha huko watakakofika kuwa tayari zoezi limeshawafikia, hivyo wasihesabiwe tena,” ameongeza.
Aidha Makinda amewataka watu wote wenye vitambulisho vya aina yoyote kuviandaa mapema ili kuhakikisha hawacheleweshi zoezi zima mara vinapohitajiwa na karani.
“Tunatamani watu wote wenye vitambulisho vyovyote waviandae waviweke karibu ili kueopuka kupoteza muda wakati wa tukio ili pale karani atakapoomba Kitambulisho mtu asiende ndani na kuanza kukitafuta kwa muda mrefu. Lakini sio kwamba meu hatahesabiwa asipokuwa na kitambulisho, Hapana wote watahesabiwa ila tunataka kujua wangapi wanavyo na wangapi hawana ili tuendelee kuwaandalia.” Kamisaa wa sensa, Anne Makinda.
“Sisi tunachosema, hii tarehe 23, ni kama Roho ya nchi hivyo kila mwananchi ajiskie kama anahusika, ni muhimu sana kwa Maendeleo ya Nchi, hakuna mtu yoyote ambae anasema maswala ya siasa wala binafsi ni kwa Maendeleo yetu sote. Tunaomba kila mwananchi ajihusishe kikamilifu na ajiandae kuhesabiwa. Anne Makinda Kamisaa wa Sensa.
Sensa ya watu na Makazi inatarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka 2022 kwa lengo la kupata idadi wa watu wote na makazi kwa Maendeleo ya taifa la Tanzania.