Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa mpaka sasa limepokea barua 273 za makocha ambao wanataka kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, ambayo kwa sasa ipo chini ya kaimu kocha mkuu Etienne Ndayiragije.

Mtendaji mkuu wa benchi la ufundi, Oscar Mirambo, amesema kuwa wamepokea maombi mengi ya makocha kutoka nje ya nchi ambao wanahitaji kuinoa timu ya Taifa ya Tanzania.

“Tulitangaza nafasi kwa kocha ambaye ana uwezo wa kuinoa timu yetu na mwitikio umekuwa mkubwa kwa makocha wa kigeni, wengi wametuma barua za maombi ya kazi ikiwa ni zaidi ya barua 273, ambazo zimepokelewa hadi sasa.

“Katika maombi hayo yote ya makocha ambao wanahitaji hakuna jina la mzawa hata moja, hali ambayo inaonyesha kuwa mwamko kwao umekuwa mdogo.

“Kuhusu Ndayiragije yeye alipewa kazi ya kuvusha timu kwenye michuano ya Chan ambayo inawahusisha wachezaji wa ndani kufanikiwa hilo ameliweza, kilichobaki ni kupokea ripoti na kuifanyia kazi mambo mengine yatafuata kujua hatma yake kwani siyo suala la kukurupuka,” alisema Mirambo.

Wakurugenzi watakiwa kupambana na malaria
Serikali yaonya matangazo ya dawa mtandaoni