Uongozi wa chama cha soka nchini Argentina (AFA) umewatangaza Lionel Scaloni na Pablo Aimar kuwa makocha wa muda wa timu ya taifa ya nchi hiyo, baada ya kuvunja mkataba na kocha Jorge Luis Sampaoli Moya, mwezi uliopita.
AFA imewateua makocha hao wawili kwa kuamini wataweza kuivusha timu yao ya taifa katika kipindi hiki ambacho wanaendelea na mchakato wa kumsaka kocha ambaye atakua na wajibu wa kuiwezesha Argentina kufikia malengo iliyojiwekea katika medani ya soka.
Pablo Aimar mwenye umri wa miaka 40 ameteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Argentina chini ya umri wa miaka 17 kuanzia mwaka 2017, huku Scaloni akipandishwa kutoka kwenye kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20.
Wawili hao watakua na kazi kubwa ya kuhakikisha Argentina inapata ushindi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Colombia, utakaochezwa mjini Guatemala mapema mwezi ujao.
Endapo Lionel Messi na baadhi ya wachezaji wataendelea na mpango wa kuitumikia timu ya taifa, tofauti na matarajio ya fununu za kutangaza kustaafu, watakua chini ya makocha hao katika mchezo huo ambao utakua wa kwanza baada ya Argentina kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia zilizofanyika Urusi wakiishia hatua ya 16 bora.
Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora, Argentina ambao hawakuwa na ushawishi wa kuleta upinzani wakati wa fainali za kombe la dunia, walifungwa na Ufaransa 4-3.