Makocha zaidi ya 100 wameomba kazi ya kukinoa kikosi cha Simba SC, baada ya kuondoka kwa Kocha kutoka nchini Hispania Franco Pablo Martin mwnzoni mwa juma lililopita, kufuatia mkataba wake kuvunjwa kwa makubaliano maalum na Uongozi wa klabu hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema, baada ya kupokelewa kwa maombi ya Makocha hao 100, Uongozi wa klabu hiyo kupitia Kamati Maalum ulifanya mchujo na kubaki na Makocha 40, ili kuanza mchakato Rasmi wa kumsaka Kocha Mkuu Mpya atawasili nchini kabla ya Ligi Kuu msimu huu kufikia tamati.
“Kwa sasa kikosi kipo chini ya Kocha Msaidizi Seleman Matola, ambaye atasimamia michezo yote ya Ligi Kuu iliyosalia, lakini taratibu za kusaka Kocha mpya zinaendelea, juma lililopita tulifunga Rasmi zoezi na kupokea maombi.”
“Simba SC imepokea maombi ya Makocha zaidi ya 100 na Kamati Maalum iliketi juma lililopita ikapitia maombi hayo na kupunguza hadi kufikia Makocha 40, juma hili kabla halijamalizika Kamati itakutana tena kuangalia maombi hayo 40 ili kuyapunguza tena, ili kubaki na idadi chache, ambayo itatoa nafasi kwa wahusika kuanza kufanyiwa usahili.”
“Atakakayekidhi vigezo vya klabu yetu katika usahili, atatangazwa Rasmi kuwa Kocha Mkuu Mpya wa klabu yetu tayari kwa kuanza kazi ya kufanya usajili na maandalizi ya kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya kimataifa.”
“Kocha atakayetangazwa pia atapata nafasi ya kuitazama timu yake katika michezo kadhaa kabla ya kufikia ukingoni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ili apate kuona aina ya wachezaji waliopo, apate kuona aina ya timu iliopo, halafu baada ya Ligi kufikia ukingoni, tutakaa naye ili aeleze mpango kazi wake.” Amesema Ahmed Ally