Miezi michache baada ya jaribio la kumuua Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kikosi kipya cha makomando kilichoteuliwa kumhakikishia ulinzi kimeonesha uwezo wake hadharani.
Kikosi hicho maalum ambacho kimekamilisha mafunzo maalum ya kuwalinda viongozi waandamizi wa Serikali pamoja na familia zao, kimeonesha uwezo wake wa hali ya juu wa kuimudu kazi hiyo na picha za mazoezi yao zimeiteka mitandao nchini humo.
Mazoezi hayo yalishuhudiwa na Waziri Mkuu mwenyewe ambaye kwa mujibu wa ofisi yake aliridhishwa sana na uwezo wa askari wa kikosi hicho maalum.
Abiy ambaye amefanya mabadiliko makubwa ya kidemokrasia na uchumi nchini humo, amefanikiwa kupata watu wengi wanaomuunga mkono lakini pia amekuwa na maadui wengi.
Wiki iliyopita, Mahakama ya kijeshi iliwafunga wanajeshi 66 ambao walituhumiwa kufanya maandamano hadi Ikulu kwa lengo la kutaka kumdhuru Waziri Mkuu. Tukio hilo liliripotiwa Oktoba mwaka huu ambapo kiongozi huyo alifanikiwa kuwatuliza wanajeshi hao na kuwaamuru wapige push up pamoja naye huku wakicheka pamoja.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Abiy alilihutubia bunge na kueleza kuwa alijawa na hofu kuona wanajeshi wengine wakiwa na silaha wameandamana hadi kwenye makazi yake. Alieleza kuwa ingawa alikuwa anacheka nao, moyoni alikuwa amejaa hofu na taharuki.
Hivi sasa, atalindwa na kikosi maalum ambacho kina kazi ya kulinda Katiba ya nchi pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali. Kikosi hicho kilijinoa zaidi kwa kipindi cha miezi sita, na jana kilionesha hadharani matokeo ya mafunzo hayo.