Syria imeshambuliwa tena kwa makombora mazito upande wa Kaskazini ambapo majeshi ya Serikali yakisaidiana na vikosi vya Iran yameweka ngome yao huku ikiaminika kuwa kuna maghala ya silaha.
Hili ni shambulizi la pili kuripotiwa baada ya lile lililofanywa wazi na Marekani na washirika wake Ufaransa na Uingereza, ambapo zaidi ya makombora 100 yalifyatuliwa.
Serikali ya Syria imeeleza kuwa katika shambulizi hilo la Jumapili, maeneo la Hama na Aleppo yalishambuliwa zaidi, lakini haikuweka wazi madhara yaliyowakuta binadamu.
Hata hivyo, kundi la wafuatiliaji kutoka Uingereza limeeleza katika ripoti yake kuwa wanajeshi 26 wanaoiunga mkono Serikali ya Syria waliuawa na kwamba wengi wao walikuwa wa Iran.
Ingawa bado haijaripotiwa rasmi nani alitekeleza tukio hilo, Israel imetajwa kuwa huenda ikawa ndiyo iliyoongoza mashambulizi hayo.
Hivi karibuni, Israel ilidai kuwa ilishambulia kambi ya jeshi la Syria katika eneo la Homs ambalo limeripotiwa kuwa ni eneo muhimu la kituo cha Iran cha kuongozea ndege zisizokuwa na rubani.