Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye anatajwa kuwa moja kati ya wakuu wa mikoa wanaukutana na upinzani mkali pamoja na changamoto nyingi katika utendaji kazi wao, Paul Makonda ameweka wazi sababu zinazompelekea kujiamini na kujiita ‘bingwa wa vita zote’ akiamini hakuna vita dhidi yake itakayomshinda.

Makonda amekuwa akikutana na upinzani mkali wa hatua anazozichukua tangu alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na sasa Mkuu wa Mkoa ambapo hivi karibuni alitangaza kubaini uwepo wa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (mashoga) 150 wanaopanga njama ya kumuangusha na kwamba ameshaanza kuwashughulikia.

Akizungumza hivi karibuni katika tamasha la uzinduzi wa Albam ya injili ya ‘Ipo Siku/Ubarikiwe ya mwimbaji Goodluck Gozbert lililofanyika Upanga jijini Dar es Salaam, Makonda alisema kuwa siri kuu ya kujiita ‘Bingwa wa vita vyote’ ni uwepo wa ‘Roho Mtakatifu’ ndani yake.

“Kama kuna mtu alikuwa na anapigwa vita nyingi ni mimi. Lakini unaweza kujiuliza ni wapi napata kiburi cha kusema kuwa ‘mimi ni bingwa wa vita vyote’. Siri ni Roho Mtakatifu aliye ndani yangu,” alisema Makonda.

Alisema kuwa amekuwa akimtumaini Mungu wakati wote na Roho Mtakatifu amemsimamia na kushinda vita nyingi dhidi yake.

Katika hatua nyingine, Makonda alisema kuwa amekuwa akiguswa na wimbo wa ‘Nikumbushe Wema Wako’ wa mwimbaji Angel Bernard na kwamba anahisi kama ametungiwa yeye wimbo huo, huku akinukuu mistari michache ya wimbo huo inayosema ‘umenikung’uta mavumbi na kuniheshimisha’.

“Huwa nahisi mtunzi wa wimbo huo alikuwa ananiongelea mimi. Kama kuna mtu amekung’utwa mavumbi na kuheshimishwa na Mungu ni mimi Paul Makonda,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi wote kutoyumbishwa na badala yake kumtegemea Mungu na kufanya kazi ili wainue vipato vyao. Baada ya maelezo yake, Makonda alipiga magoti na kuombewa na wahudhuriaji wa tamasha hilo.

Video: 'Jeshi la Polisi halikutenda haki kupiga marufuku mikutano ya Vyama pinzani' - LHRC
Exclusive: Stand Utd Kampuni Waishangaa TFF