Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa uwezo mkubwa wa Rais Dkt. Magufuli na Demokrasia ya kweli ni jambo ambalo linawavutia wageni kuja Tanzania akiwepo Rais wa Rwanda, Paul Kagame anayetarajiwa kuwasili nchini Jumapili.
Ameyasema hayo akiwa katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam baada ya kuagana na Rais Dkt. Magufuli ambaye ameelekea visiwani Zanzibar kushiriki sherehe za maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Amani Demokrasia ya kweli, upendo na uwezo wa mkubwa wa Rais Magufuli ndiyo msingi wa kuwavuta wageni kuja kutembelea hakuna mgeni ambaye anaweza kutembelea nchi ambayo haina upendo, amani na mshikamano. Tanzania chini ya uongozi wa Rais Magufuli inaendelea kuchanja mbuga katika nyanja za kidemokrasia hasa pia katika uwanja mwingine wa kidiplomasia na kuwafanya wageni waone sehemu nzuri ya kuja kutembelea,”amesema Makonda
Hata hivyo, Mbali na hilo Makonda amesema kuwa Rais Paul Kagame atawasili nchini siku ya Jumapili ya tarehe 14 ambapo atakuwa nchini kwa ziara ya siku moja na kufanya mazungumzo na Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.