Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo akizindua Ghala na Mitambo ya Gesi ya LPG ya Taifa Gas Tanzania Limited amemruhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kwenda nchini Misri kuwapa motisha wachezaji wa Taifa Stars na kuhakikisha wanapata ushindi mara baada ya kupoteza mchezo wao mmoja dhidi ya Senegal kwa kupachikwa mabao mawili kwa bila.
“Makonda umesema ukienda Misri Taifa Stars tutashinda kutokana na motisha ya ushangiliaji, panda ndege nenda si umesema tutashinda nenda” amesema Rais Magufuli.
Hadi sasa Tanzania kwenye kundi C alilokuwa amepangwa bado ana mechi mbili ambapo anatarajia kukabiliana na Kenya na Algeria.
Makonda amesema mapema leo aliweza kuwasiliana na baadhi ya wachezaji wa taifa stars akiwemo nahodha Mbwana Sammata ambaye amemuahidi kuwa mechi zinazokuja wamejiandaa vyema na kuhakikisha wanapata ushindi.
“Vijana walikata tamaa kabisa na nimeongea nao jana usiku na leo asubuhi nimeongea na Sammata, nimewaambia tumuoneshe Mh.Rais ya kwamba tupo pamoja naye,hata kama tumedondoka na Senegal lakini tunanyanyuka na Wakenya lazima watakiona na wamenihakikishia Wakenya hawatoki,”.amesema Makonda.
Aidha mchuano huo mgumu dhidi ya Taifa Stars na Senegal uliweza kushuhudiwa na wabunge 35 pamoja na muhamasishaji Pierre Likwidi ambao walirejea jana kutoka Misri wakiwa na maoni mbalimbali baada ya kuutazama mchezo huo mubashara.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amesema anakerwa na baadhi ya watanzania wanaowabeza wachezaji wa Taifa kwani wamepiga hatua kubwa ya kwenda kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya AFCON 2019 ambapo kwa muda mrefu miaka 30 iliyopita hatukuweza kupata fursa hiyo.
Ameendelea kuwatia moyo wachezaji wa Taifa na kuwahakikishia kuwa wakifanya jitihada zaidi watafanya vizuri kwa mechi zilizobakia.