Mchekeshaji maarufu nchini, Emmanuel Matebe Mathias maarufu kama MC Pilipili ametoa shukrani za dhati kwa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kwa ushirikiano alioutoa kwa kiasi kikubwa kwenye msiba wa Agness Gerald Waya maarufu kama Masogange, uliofanyika leo nyumbani kwao Mbeya.
Mc Pilipili amesema Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam ndiye aliyefanikisha safari nzima ya wasanii kwa kuwakodishia na kuwalipia magari ambayo yametumika kuwapeleka wasanii jijini Mbeya kushiriki katika mazishi ya Masogange.
Pia ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amoss Makalla kwa kuwa bega kwa bega na wasanii hao tangu kuanza kwa msiba huo mpaka mazishi yake, na amesema ameona mkono wa Serikali katika kufanikisha safari ya mwisho ya Masogange ametoa shukrani za dhati na amesema wanathamini sana mchango wao katika hilo.
“Mkuu wa mkoa wa Mbeya kuna upendo mkubwa ambao tumeuona kutoka kwenu kwani ulikuwa karibu na sisi muda mwingi, ulikuwa ukitupigia simu kujua tupo wapi hivyo naamini usiku wa leo hujalala kabisaa. Pia tunamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwani yeye ndiye aliyelipia magari mawili, matatu ambayo yametuleta hapa Mbeya leo kutokea Dar es Salaam, hata kamati ambayo ilikuwa imeandaa kuanzia kutoa heshima ya mwisho pale Leaders Club ambayo ilikuwa chini ya Steve Nyerere ilipewa nguvu na watu wa serikali tumeona serikali mmetupa support vizuri” alisema MC Pilipili
Mbali na hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ametoa neno la shukrani kwa wasanii na watu mbalimbali ambao wameweka tofauti zao pembeni na kuungana kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha wanampumzisha salama mwenzao katika nyumba ya milele.
Mueendelee kuwa pamoja hivi hivi bila kujali tofauti zenu, mabifu yenu mzidi kuwa wamoja kwani hili jambo mmejenga heshima kubwa sana, naomba nitoe pole sana kwa familia kwa msiba huu” alisema Makalla