Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa kuna ofisi ameibaini ilichangisha fedha kwaajili ya Taifa Stars lakini wakazitumia kwa shughuli zao na wengine kwa shughuli za kitalii.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam mara baada ya kuwasili kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) ikitokea nchini Misri ilikokuwa imeenda kwaajili ya mashindano ya mpira wa miguu wa mataifa ya Afrika (AFCON)
Makonda ameitaka ofisi hiyo ambayo hakuitaja kuzipeleka fedha hizo kwenye akaunti maalum iliyotangazwa na waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ili ziweze kuwasaidia wachezaji na si vinginevyo.
”Kuna jambo nimelibaini nilipokwenda Misri, ipo ofisi moja iliyochangisha fedha kwa ajili ya Taifa Stars lakini wakazitumia kwa matumizi yao na wengine kutumia kwa shughuli za utalii, hizo fedha nazitaka, vinginevyo wazipeleke BMT,”amesema Makonda
Aidha, ameongeza kuwa kuna baadhi ya Watanzania ambao walikuwa wakiiombea kufanya vibaya Taifa Stars katika michuano hiyo, wakizani kuwa wanamkomoa yeye huku wakisahau kuwa ile timu ni ya taifa.
Hata hivyo, Makonda amehimiza umoja na mshikamano wa kuisaidia timu ya taifa, kwani bado inakabiliwa na mashindano mengine ya CHAN, yanayohusisha wachezaji wa ndani ya bara la Afrika.