Wakati chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wote wenye umri chini ya miaka 14 ikitarajiwa kuanza kutolewa Jumatatu wiki ijayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ana mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba kuwapima wanaume saratani tezi ya dume.
Makonda ameyasema hayo leo Aprili 21 wakati akifungua rasmi warsha ya chanjo hiyo iliyowashirikisha waandishi wa habari, wataalamu wa afya, viongozi mbalimbali wa dini na siasa.
“Kuna kasumba kuwa saratani ya tezi dume inapimwa kwa kidole jamani siyo kweli, kuna kipimo cha damu na ni rahisi hivyo nina mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba katika mkoa wangu kuhakikisha hii kasi ya vifo kwa kinababa inapungua kwa kuwagundua mapema na kuwaanzishia matibabu,” amesema Makonda.
Amesema wakati saratani ya mlango wa kizazi ikiwaathiri wanawake nchini, tezi dume inaumiza zaidi akina baba ambao hata hivyo hakuna mwamko wa kulizungumzia jambo hilo katika jamii.
Pia, ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali za mitaa na viongozi wa dini kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wasichana wote wenye umri huo wafike kwenye vituo kwa wingi kupata chanjo.
Makonda amesisitiza pia kuzingatia kupata chanjo kamili kwa kurudi mara ya pili ili kuikamilisha.