Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa hawezi kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa hajapokea barua ya kuitwa.
Aidha, Bunge lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla halija ahirishwa lilipitisha azimio la kumtaka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexender Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa kutokana na kauli zao walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa dola.
”Hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti, sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huo na sijaletewa barua rasmi,”amesema Makonda.
Aidha, baada ya Bunge kufikia uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge iwaandikie barua viongozi hao, baadhi ya wabunge walihoji kauli ya Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah kwamba azimio la chombo hicho cha kutunga sheria kumtaka Makonda kufika katika kamati hiyo kujieleza kuhusu tuhuma za kuudharau mhimili huo hazijafuata utaratibu.
Kwa upande wake Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na mwenzake wa Iringa Mjini Peter Msigwa (Chadema), walihoji kauli ya Kashililah ya kukosoa uamuzi huo wa kutotekelezwa kwa azimio hilo.