Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Africana Kinzudi yenye urefu wa Kilometer 3.3 ambayo ujenzi wake utagharimu zaidi ya Shilingi Million 900.
Ujenzi wa Barabara hiyo kwa kiwango cha lami inaenda sambamba na uwekaji wa matuta, mitaro ya maji, taa za barabarani, Calvert na alama za watembea kwa miguu ambapo itajengwa na TARURA.
Baada ya kuzindua Barabara hiyo Makonda amefanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Kata za Wazo na Mbezi Juu uliolenga kupatia majibu ya changamoto zinazowakabili kwenye sekta ya Miundombinu, Elimu, Afya, Maji, Ardhi na Usafiri ambapo wakazi wa Kata hizo wamefurahia kuona kero zao za muda mrefu zimepatiwa ufumbuzi wa haraka.
Katika mkutano huo Makonda ameelezea miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa kwaajili ya usafiri wa treni kutoka Wazo kuelekea Mwenge, Airport na Posta ambayo itasaidia usafiri na kupunguza msongamano wa magari.
Aidha, Makonda amewataka wananchi waliojenga kwenye hifadhi ya barabara ya Afrikasana Kinzudi kushirikiana na serikali kuhakikisha ujenzi unafanikiwa huku akiwataka wakazi waliojenga ndani ya hifadhi ya bomba la Maji kutokea Ruvu kushirikiana kwa kina na DAWASA.
Pamoja na hayo, Makonda ameagiza kila mtaa kuwa na Ramani ya mipango miji ili kukabiliana na migogoro ya ardhi na utapeli ambapo pia amewataka wananchi waliocheleweshewa kupatiwa vibali vya ujenzi kufika ofisini kwake Julai Mosi.