Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameagiza mgambo waliopiga raia katika eneo la Bunju A kuchukuliwa hatua kali kwani walichokifanya haukuwa mpango wa mkoa.

Makonda amekemea vikali kitendo hicho amabacho kimefanyika kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Bunju ambapo Mgambo hao wamepiga raia na kuwajeruhi akiwemo mfanyabiashara, Robson Orotho mkazi wa Bunju kutokana na kushindwa kulipa Sh. 50,000 ya taka.

”Nimeshtuka sana baada ya kuona video hiyo sio kitendo cha kufanywa na watendaji kwani lengo letu ni kusimamia usafi na si kupiga raia, nalaani kitendo hicho na naagiza hatua kali zichukuliwe dhidi yao,” amesema Makonda.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limethibitisha kuwashikilia mgambo watatu wa Manispaa hiyo ambao wamehusika katika tukio hilo na taratibu za kisheria zinaendelea na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Aidha, Kamanda Murilo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Goodluck Festo, Rehema Nyange na Kelvin Edson, ambao wote ni Mgambo wa Manispaa hiyo huku akibainisha kuwa mfanyabiashara huyo anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala.

Hata hivyo, siku za hivi karibuni zimesambaa picha za video katika mitandao ya kijamii zikionyesha mgambo wakitoa kipigo kwa watu na kuzua taharuki, wengi wakiwa ni wafanyabiashara ndogo ndogo

Watanzania 27 wakamatwa nchini Kenya
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 1, 2018