Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ameibuka na kusema kuwa hababaishwi na kelele za watu juu ya mapambano yake dhidi ya dawa za kulevya na kuapa kuendelea kuwanyoosha.
Aidha, amesema kuwa kushambuliwa kwake na baadhi ya watu wasioutakia mema mkoa wa Dar es salaam, kuna lenga kupoteza vita dhidi ya dawa ya kulevya, lakini kamwe kelele hizo haziwezi kumtoa katika reli ya vita hiyo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kigamboni, amesema kuwa Dar es salaam ilikuwa kama chuma kilichokuwa kimepinda na kuwa kinachofanyika sasa hivi ni kukinyoosha na kitanyooka tu.
“Waache waongee sana katika mitandao ya kijamii, sitarudi nyuma, nitawanyoosha tu tupo katika kipindi cha mpito, hivyo lazima kelele nyingi zitasikika,”amesema Makonda.
Hata hivyo amesema kuwa haiwezekani taifa liendelee kutumia fedha nyingi katika kutibu waaathirika wa dawa za kulevya, nbguvu kazi ya vijana inahitajika hivyo vijana nao wanatakiwa wajifunze kwa wenzao walioacha kutumia dawa hizo.