Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kasi ya maendeleo inayoshuhudiwa katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imesababisha mabishano kwenye mitandao kuhusu muda aliokaa madarakani.
Ameeleza kuwa yeye pamoja na watu wengine wamekuwa wakijaribu kuwaelewesha baadhi ya watu kuhusu kipindi ambacho Serikali hii imekaa madarakani tangu ilipochaguliwa mwaka 2015, ambao wamechanganywa na maendeleo wanayoyaona.
“Mabishano yetu ni kwamba wewe umekaa madarani miaka saba. Na sisi tunajaribu kuwakumbusha kuwa sio miaka saba ni miaka mitatu. Tunabishana kwa sababu kasi ya maendeleo inafanana na mtu aliyekaa madarakani zaidi ya miaka saba,” alisema Makonda.
-
Ndege ya kisasa mpya ATCL kutua nchini, JPM kuipokea
-
Bashiru Ally awataka CCM kumuunga mkono Lwakatare
Makonda ambaye leo alipewa nafasi ya kusema neno katika mapokezi ya ndege mpya Airbus 220 – 300, mbele ya Rais Magufuli na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, alieleza kuwa ujenzi wa daraja la juu, reli ya kisasa (SGR), kufufua Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na mambo mengine ndani ya muda mfupi ndio chanzo cha mjadala huo.
Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamewaongoza Watanzania kuipokea ndege hiyo mpya katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.