Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Urusi Vladmir Putin bado hawajafikia maelewano kuhusu mzozo unaoendelea ambao umesababishwa na hatua ya Urusi kuwapeleka maelfu ya wanajeshi karibu na mpaka wake na Ukraine.
Baada ya mazungumzo ya masaa mawili kwa njia ya video hapo jana, Biden amemuonya Putin kuwa atawekewa vikwazo vikali vitakavyokuwa na athari kubwa kwa uchumi endapo Urusi itaivamia tena Ukraine.
Aidha Mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani Jake Sullivan amesema Biden amemwambia Putin kuwa Marekani itasimama na Ukraine pamoja na washirika wake katika upande wa Ulaya.
Naye mshauri wa Putin kuhusu mambo ya kigeni Yuri Ushakov amesema Rais Putuin huyo amemwambia Biden kuwa vikosi vya Urusi vipo kwenye mpaka wake, na havimtishii yeyote. Viongozi hao pia wamejadili mpango wa nyuklia wa Iran na mashambulizi ya mtandaoni.