Shirika la Umoja wa Mataifa la ukaguzi wa nyuklia IAEA limefikia makubaliano na Iran kuhusiana na kuvifanyia marekebisho vifaa vya ukaguzi kwa ajili ya kuendesha shughuli zake.
Suala hilo lilikuwa ni la dharura na suluhisho hilo lililopatikana linaleta matumaini ya mazungumzo mapya ya mkataba wa nyuklia na mataifa ya Magharibi.
Mkuu wa shirika hilo Rafael Grossi alipata makubaliano hayo katika ziara ya dakika ya mwisho ya Tehran kabla ya kufanya mkutano na magavana wa IAEA wiki hii ambapo nchi za Magharibi zenye nguvu zilikuwa zinatishia kutafuta suluhisho la kuikosoa Iran kwa kulizuia shirika hilo kutekeleza majukumu yake.
Suluhisho hilo lilikuwa na hatari ya kuzidisha mvutano baina ya Iran na Marekani ambao ungekuwa kikwazo kwa mazungumzo ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na Marekani.