Watu 40 wamepoteza maisha kwenye msongamano wa umati mkubwa uliokuwa ukitembea katika jiji la Kerman kuupokea mwili wa Kamanda wa Jeshi la Iran, Qassem Soleimani aliyeuawa na Marekani.
Kwa mujibu wa Fars News, watu 213 wameripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo, mapema leo, Januari 7, 2020.
Awali, mkuu wa kitengo cha huduma za dharura wa Iran, Pirhossein Koolivand alikiambia kituo cha televisheni cha taifa hilo kuwa watu 32 walikuwa wamepoteza maisha na wengine 190 walijeruhiwa kutokana na umati mkubwa uliopitiliza.
Video zilizokuwa zimesambaa mtandaoni, zilionesha baadhi ya waombolezaji wakiwa wamelala barabarani na wengine wakijaribu kuwaokoa, huku vilio na yowe vikitawala.
Maelfu ya watu walikusanyika katika jiji la Kerman kwa ajili ya kumzika Kamanda Qassem Soleimani, Kiongozi wa jeshi maalum la Ukombozi la Iran linalojulikana kama ‘Quds’.
Aliuawa Ijumaa iliyopita kutokana na shambulizi la Marekani la kutumia ndege isiyo na rubani, karibu na uwanja wa kimataifa jijini Baghdad, nchini Iraq.
Hata hivyo, ratiba ya mazishi imebadilishwa ghafla, na bado tarehe nyingine haijatolewa lakini umati wa watu unazidi kumiminika katika barabara zilizotajwa kuwa mwili huo utapita.
Serikali ya Iran imetangaza kulipa kisasi kwa kushambulia Marekani na washirika wake, huku Rais wa Marekani Donald Trump akitahadharisha kuwa wakifanya jaribio lolote la kulipa kisasi jeshi lake litapiga maeneo 52 ya Iran ikiwa ni pamoja na maeneo nyeti.