Watu tisa wamefariki Dunia na wengine sita wameokolewa wakiwa hai baada ya Boti iliyobeba Watu takribani 30 kuzama Baharini Kisiwani Pemba wakati Watu hao wakitokea Chakechake kwenda Kisiwa Panza kwenye shughuli za mazishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Richard Mchomvu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema hadi usiku wa Januari 4, miili tisa ya waliofariki imeopolewa kwenye maji na Watu sita wameokolewa wakiwa hai.
“Boti la kwanza ambalo lilibeba mwili wa Marehemu lilivuka salama lakini nyingine ambalo lilikuwa na Watu (Ndugu wa Marehemu na Waombolezaji wengine wanaokisiwa kufikia 30) likapata shida Baharini na likazama,” alisema.
“Mpaka sasa waliookolewa sita wote ni wanaume na maiti tisa zilizoopolewa zote za Wanaume Watu wazima,” RPC Mchomvu.
RPC Mchomvu amesema kutokana na giza, zoezi la uokozi litaendelea asubuhi kwa sababu kuna Watu bado wapo kwenye maji.
Hata hivyo kwa tofauti ya masaa takribani 7 watu wamezua mijadala wakihoji endapo bado waokoaji watawakuta hai watu waliosalia baharini.