Klabu ya Tottenham ya nchini England imepangwa kundi moja na mabingwa wa soka Hispania FC Barcelona katika mshike mshike wa ligi ya mabingwa barani Ulaya ambao utaanza rasmi mwezi Septemba.

Wawili hao wamekutanishwa kupitia upangaji wa makundi uliomalizka jioni hii kwa saa za Afrika mashariki, mjini Monaco- Ufaransa, ambapo klabu 32 zilizofuzu kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo zimefahamu wapi zilipoangukia.

Mbali na FC Barcelona kikosi cha Mauricio Pochettino, pia kitakutana na PSV ya Uholanzi pamoja na Inter ya Italia, katika michezo ya kundi B.

Mashetani Wekundu (Manchester United) nao wameangukia katika kundi gumu kwenye mchuano hiyo, baada ya kupangwa na mabingwa wa nchini Italia Juventus FC, Valencia (Hispania) na Young Boys (Uholanzi) katika kundi H.

Hatua ya Man utd kupangwa kundi moja na Juventus FC, itamuwezesha mshambuliaji bora duniani kwa sasa Cristiano Ronaldo kurejea kwa mara nyingine kwenye uwanja wa Old Traffod, ambao kwa mara ya mwisho alicheza dhidi ya Mashetani hao, akiwana Real Madrid.

Washindi wa pili wa michuano hiyo msimu uliopita, Majogoo wa jiji Liverpool wameangukia mikononi mwa mabingwa wa Ufaransa PSG, SCC Napoli (Italia) na Crvena Zvedza (Serbia) katika kundi C.

Kwa upande wa mabingwa wa soka nchini England Manchester City wamepangwa katika kundi F, sambamba na Shakhtar Donetsk (Ukraine), Lyon (Ufaransa) na Hoffenheim (Ujerumani).

Nao mabingwa watetezi wa michuano hiyo Real Madrid watapambana na wapinzani wao katika hatua ya nusu fainali msimu uliopita AS Roma katika michezo ya kundi G, ambalo linazijumuisha klabu za CSKA Moscow (Urusi) na Viktoria Plzen (jamuhuri Ya Czech).

Makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu wa 2018/19.

Kundi A: Atletico Madrid, Borussia Dortmund, Monaco, Club Brugge.

Kundi B: Barcelona, Tottenham, PSV Eindhoven, Inter Milan.

Kundi C: Paris St-Germain, Napoli, Liverpool, Red Star Belgrade.

Kundi D: Lokomotiv Moscow, Porto, Schalke, Galatasaray.

Kundi E: Bayern Munich, Benfica, Ajax, AEK Athen.

Kundi F: Manchester City, Shakhtar Donetsk, Lyon, Hoffenheim.

Kundi G: Real Madrid, Roma, CSKA Moscow, Viktoria Plzen.

Kundi H: Juventus, Manchester United, Valencia, Young Boys.

Michezo ya hatua ya makundi imepangwa kuchezwa Septemba 18–19, Oktoba 2–3, 23–24, Novemba 6–7, 27–28 na Disemba 11–12 2018.

Michezo ya hatua ya 16 bora mkondo wa kwanza imepangwa kuchezwa Februari 12, 13, 19 na 20, na mkondo wa pili itachezwa Machi 5, 6, 12 na 13, 2019.

Michezo ya hatua ya robo fainali mkondo wa kwanza itachezwa Aprili 9 na 10, na mkondo wa pili itaunguruma Aprili 16 na 17, 2019

Michezo ya hatua ya nusu fainali mkondo wa kwanza itachezwa Aprili 30 April na Mei 1, na mkondo wa pili itachezwa Mei 7 na 8, 2019

Mchezo wa fainali utaunguruma Juni Mosi 2019, kwenye uwanja wa Wanda Metropolitano mjini Madrid- Hispania.

Luka Modric mchezaji bora Ulaya
Southgate atangaza jeshi litakaloivaa Hispania, Uswiz