Mapigano kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Jamhuri ya Kimdemokrasia ya Congo (DRC), yamesababisha watu wengi kuhama makazi yao katika eneo la Rutshuru lililopo jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini, huku Watoto wengi wakipotezana na Wazazi wao.
Kwa mujibu wa shuhuda mmoja Maniraguha Nzabagasani ambaye anaishi anaishi katika majengo ya shule ya Nyiragongo, amesema analazimika kuishi hapo na baadhi ya watoto asiowajua na kwamba wa kwake akiwa hajui walipo.
Justine Nzabahariye, mama mmoja katika eneo la jirani na Goma amesimulia kuwa risasi zilikuwa zikivuma kiasi cha kuwalazimu kukimbia kutafuta usalama wao kitu kilichosababisha watoto wake hao wawili kupotea na kwamba anawaombea kwa Mungu awalinde popote walipo.
“Mtoto wangu alikuwa amelala kwa majirani ghafla asubuhi na mapema saa 3 asubuhi kulisikika milio ya risasi, tukakimbia na wale niliokuwa nao na sijamuona yeyote na sijui kama wapo hai ila namuomba Mungu awalinde mahala walipo,” amehuzunika mama huyo Nzabahariye.
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), imethibitisha kuwa watoto kadhaa wametenganishwa na familia zao, huku Mkuu wa ujumbe mdogo wa ICRC/Goma, Raphael Tenaud akisema takwimu za kupotea watoto zimekuwa ni za kutisha.
“Zaidi ya watoto 800 hadi sasa hawana uangalizi na wamewapoteza wazazi wao, wamepoteza familia zao, hawa ni watoto ambao wamejikuta wakihamishwa na watu wasiowafahamu na ambao sasa wanawafuatiliwa wazazi wao,” amesema Tenaud.
Kwa mujibu wa UNICEF, tangu mwisho wa mwezi Machi, zaidi ya watu 158,000, nusu yao wakiwa ni watoto, wamekimbia makazi yao katika maeneo ya Rutshuru kufuatia kushamiri kwa mapigano ya silaha.