Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria na kwa kushirikiana na Wadau pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatekeleza Mpango Mkakati wa Malaria wa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Ummy ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2023 ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya mnazi mmoja vilivyopo Jijini Dar es Salaam.
Amesema, “mkakati wa udhibiti wa mbu waenezao malaria unatekelezwa kupitia afua kuu nne za ugawaji na matumizi ya vyandarua vyenye dawa, upuliziaji viuatilifu ukoko kwenye kuta ndani ya nyumba, utunzaji na udhibiti wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu pamoja na unyunyiziaji wa viuadudu vya Kibaiolojia kwenye mazalia ili kua viluwiluwi vya mbu.”
Aidha, Waziri Ummy amesema mpango mkakati huo unalenga kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini kutoka wastani wa asilimia 7.5 ya mwaka 2017 hadi kufikia wastani wa chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025.