Mshambuliaji mpya wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona Malcom amesisitiza kupambana ili kufanikisha lengo la kuingia kwenye kikosi cha kwanza, baada ya kucheza mchezo wa kombe la Mfalme usiku wa kuamkia jana dhidi ya Leonesa.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Brazil mwenye umri wa miaka 21, alicheza mchezo huo wa kwanza tangu aliposajiliwa klabuni hapo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi akitokea klabu ya Bordeaux ya Ufaransa, kwa ada ya Euro milioni 41.
Malcom aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo ulioshuhudia FC Barcelona wakiibuka na ushindi wa bao moja kwa sifiri, anajihisi furaha kuwa sehemu ya kikosi, na hana budi kupambana ili kuendelea kumshawishi meneja hadi kuingia kwenye kikosi cha kwanza.
“Sina budi kumshukuru meneja kwa kunipa nafasi kwa mara ya kwanza, nitaendelea kupambana katika mazoezi ya kila siku, ili nifikie lengo la kuingia kwenye kikosi cha kwanza.”
“Lengo langu ni kucheza katika kikosi cha kwanza, hakuna litakalo shindikana kwa sababu nipo, na nitaendelea kuwepo klabuni hapa, kama lengo la usajili lilivyokusudia.” Alisema Malcom.