Klabu ya AS Roma imekubali kumsajili mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Brazil na klabu ya Girondins Bordeaux ya Ufaransa Malcom Filipe Silva de Oliveira.
Makubaliano ya klabu hizo mbili yameafikiwa, huku pande zote mbili zikiendelea kufanya siri ada ya uhamisho wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21.
Hata hivyo baadhi ya vyombo vya habari vya Italia vimeripoti kuwa, Malcom ameihama Girondins Bordeaux kwa ada ya Euro milioni 37, sawa na Pauni milioni 33.
“Klabu inathibitisha kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji Malcom kutoka FC Girondins de Bordeaux, mchezaji huyu atafanyiwa vipimo vya afya na kusaini mkataba ndani ya juma hili,” imeeleza taarifa iliyotolewa na uongozi wa AS Roma.
“Mshambuliaji huyu kutoka Brazil, atawasili mjini Roma wakati wowote, na atakamilisha taratibu zote za uhamisho wake.”
Malcom alijiunga na Bordeaux mwezi Januari 2016 akitokea nchini kwao Brazil alipokua akiitumikia klabu ya Corinthians, na mpaka anathibitishwa kuondoka nchini Ufaransa tayari alikua ameshacheza michezo ya Ligue 1, 96 na kufunga mabao 23.
Vyombo vya habari vya England juma lililopita viliripoti kuwa, klabu ya Everton ilikua tayari kumsajili Malcom, huku klabu nyingine kutoka nchini humo Tottenham Hotspur ilikua ikimfuatilia na iliweka mipango ya kumsajili kabla ya kumsajili Lucas Moura aliyetokea Paris St Germain mwezi Januari mwaka huu.
Malcom anakua mchezaji wa tisa kusajiliwa na meneja wa AS Roma Eusebio Di Francesco, akitanguliwa na Javier Pastore, Justin Kluivert, Davide Santon na Bryan Cristante.