Mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU), inamshikilia Rais wa shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi na katibu mkuu wake, Celestine Mwesigwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi.
Taarifa zinaeleza kwamba viongozi hao wa TFF wamekamatwa usiku wa kuamkia leo Juni 28, 2017 na wanahojiwa na TAKUKURU kwa tuhuma hizo.
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tuhuma mbalimbali dhidi yao kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Taasisi hiyo ya kitaifa ambapo taarifa zinaeleza kuwa inasemekana TAKUKURU wamekuwa kwenye uchunguzi kwa muda sasa, mpaka jana walipoamua kuwatiwa nguvuni.
Aidha, gazeti la Nipashe hivi karibuni liliandika mfululizo wa makala zilizokuwa zikielezea tuhuma za ufisadi ndani ya TFF na tuhuma hizo zilielekezwa kwa Malinzi na viongozi wenzake wa shirikisho hilo.
Moja ya makala zilizoandikwa ni hii iliyopewa kicha cha habari “JAMALI AMEFANYA HAYA UFISADI WA KUTISHA TFF”
Na Makala hiyo ya Nipasheni iliyowekwa katika tovuti ya Shaffih Dauda imeeleza kuwa – “Ripoti ya ukaguzi wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania kwa Taifa Stars iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inaelezwa kuwa, mbali na mambo mengine, TBL iliamua kufanya ukaguzi huo ili kujiridhisha kama shirikisho linazingatia makubaliano yaliyomo kwenye mkataba.
Inaelezwa katika ripoti hiyo ambayo uongozi wa juu wa TBL uliithibitishia Nipashe jana kwamba ilifanywa na Mkaguzi Mkuu wake wa ndani, Richard Magongo, kuwa kati ya Novemba 13, 2013 (siku 11 tangu uongozi wa sasa wa TFF uingie madarakani) na Februari 15, 2014, Dola za Marekani 315,577 (Sh. milioni 688.368) zilitumika bila ya nyaraka za kuthibitisha matumizi yake kinyume cha makubaliano ya mkataba wa pande hizo mbili.
Kati ya Novemba 11, 2013 na Machi 11, 2014, Dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) pia zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaanishwa katika mkataba wa TBL na TFF, ripoti inabainisha.
Mchanganuo wa ripoti hiyo unaonesha kuwa, miongoni mwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kutumia fedha hiyo ni pamoja na rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambaye Desemba 24, 2013 alilipwa Dola za Marekani 159 kupitia vocha yenye namba 1075 zikiwa ni gharama za malazi hotelini (Hotel accommodation).
Ripoti inaonesha kuwa, siku hiyo hiyo (Desemba 24, 2013), Malinzi alilipwa na TFF Dola 10,000 kupitia vocha namba 1077 (Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya fedha za Jamal Malinzi), kisha Februari 6, 2014 akalipwa Dola 15,934 (Loan Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya mkopo kutoka kwa Jamal Malinzi) na baadaye kulipwa Dola 69,471 kupitia vocha namba 1098 na Dola 63,735 kupitia vocha namba 1401.
Wengine waliopewa fedha hiyo ya udhamini wa TBL kwa Taifa Stars ni aliyekuwa msaidizi wa Malinzi, Juma Matandika, Ali Ruvu na mwingine aliyetajwa kwa jina la S. Madadi ambao kwa pamoja walilipwa Dola 1,084 kupitia vocha namba 828 Februari 6, 2014.
Ripoti pia inabainisha malipo ya Dola 3,500 Januari 16, 2014 kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF jijini Nairobi.
Pia zimo Dola 4,630 zilizochotwa Desemba 24, 2013 kugharamia mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi (Cooper test for referees), Dola 4,120 zilizotolewa siku hiyo hiyo kwa ajili ya Ally Mayay na Ayubu Nyenzi kufanya ziara Uganda na Dola 1,638 ambazo zilitolewa siku hiyo hiyo zikiwa fidia ya malipo ya deni la TFF kulipia ziara ya uongozi wa shirikisho mkoani Mwanza.
Dola 4,023 zilitolewa Desemba 24, 2013 kwa ajili ya posho ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa wafanyakazi wa TFF na Dola 30,000 zilitumika kwa semina elekezi kwa makocha iliyofanyika Lushoto (coach retreat at Lushoto), ripoti inasema.
Inaongeza: “Dola 2,829 zilitumika kutoa rambirambi na misaada, Dola 3,298 zikakopeshwa kwa Chama cha Soka Mbeya huku Dola 989 zikitolewa kwa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara zikiwa ni msaada.”
Katika ripoti hiyo, inaelezwa kuwa, Dola 90,000 zilitumika kulipia fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na Dola 34,177 zikatumika kununua magari mawili aina ya Toyota Hiace.
Ripoti inaeleza kuwa, kulikuwa na mawasiliano rasmi kati ya maofisa wa TFF na TBL kabla ya kufanya malipo kwa Poulsen na ununuzi wa magari hayo.”