Serikali nchini, imesema tayari imewalipa wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME jumla ya Shilingi 2.43 Bilioni ikiwa ni malipo ya awali ya fidia ya bima ya amana kwa wateja 3,446, hadi mwezi Machi mwaka huu, 2023.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chwaka, Mhe. Makame Mlenge Haji, aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa waathirika wa Benki ya FBME.
Amesema, malipo hayo yamefanyika kupitia Bodi ya Bima ya Amana – DIB, kwa wateja wa Benki hiyo waliojitokeza kuidai malipo hayo na kuongeza kuwa, “malipo ya fedha za ufilisi kwa wateja wenye amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 yanayotokana na uuzaji wa mali, makusanyo ya madeni, mikopo na fedha nyingine za Benki hiyo yatafanyika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023.”
Aidha ameongeza kuwa, fedha za ufilisi zitalipwa baada ya Mahakama ya Cyprus kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na Benki Kuu ya Cyprus la kuitambua DIB kama Mfilisi wa benki ikijumuisha Makao Makuu pamoja na tawi la Cyprus, uamuzi unaotarajiwa kutolewa ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023.