Mahakama ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja chini ya uangalizi maalum, Esther Mwaniwasa baada ya kumkuta na hatia ya kumkata sehemu za siri mwanaye wa kiume mwenye umri wa siku tatu.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Ramadhani Rugemarila alisema kuwa mwanamke huyo mwenye watoto wanne, mkaazi wa kijiji cha Katuka wilayani humo alifanya kosa kinyume cha kanuni ya adhabu (penal code).
Hakimu Rugemarila alisema kuwa upande wa mashtaka ukiongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Rajab Mrisho waliweza kuthibitisha pasipo na shaka kuwa kosa hilo lilifanywa na Mwaniwasa.
Upande wa mashtaka uliliwasilisha mashahidi wanne Mahakamani hapo, na Hakimu alimtaka mwanamke huyo kuhakikisha hafanyi kosa lolote anapokuwa katika kipindi hicho maalum cha uangalizi.
Mwaniwasa aliiomba Mahakama kutompa adhabu kali kwakuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya kosa hilo. Pia, alisema ana watoto wanne wanaomtegemea, hivyo akipewa adhabu kali itawagharimu.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo tangu mwaka jana, ilielezwa kuwa Mwaniwasa alifanya kosa hilo Desemba 26, 2019 majira ya saa mbili kamili usiku katika kijiji cha Katuka.
Ilielezwa kuwa baada ya kutukio hilo, mtoto huyo alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Matai na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Rukwa iliyoko mjini Sumbawanga.