Mke wa mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Omkituri kata Kibeta katika Manispaa ya Bukoba, ameuwawa na watu ambao hawajajulikana usiku wa kuamkia leo, Juni 13, 2023.

Akizungumzia tukio hilo, mama mkwe wa marehemu Anajoyce Deus amesema akiwa nyumbani kwake majira ya saa 12 asubuhi alisikia mlio wa pikipiki kwa nje na baadae watu walibisha hodi katika nyumba ya mtoto wake ambaye ni mume wa marehemu.

Amesema, “asubuhi nilikuwa najiandaa saa 12 ili niende kazini lakini baadae kabla sijaamka kitandani nikasikia mlio wa pikipiki baadae nikaona imekuja moja kwa moja kwa mwenyekiti baadae wakakaa wakaongea huyo mama na kijana wa bodaboda,” alisema.

Aidha mama huyo ameendelea kusema kwamba, “baada ya dakika mbili wakagonga mlango na Mimi nikawa nishaamka nakuja huku baadae nikachungulia kwenye tundu la jiko kuangalia kule kwa mwanangu kuna nini, baadae nikaona mwanangu anaenda na mimi nikamfata kwa nyuma.”

“Kufika pembe ya nyumba nikasikia mwanangu analia nikakimbia kufika pale nikakuta shingo amelala hivi wadudu wameshampanda sasa mwanangu akasema mama huyu ameshakufa,” alisimulia mama huyo.

Meya wa manispaa ya halmashauri ya Bukoba, Godson Gibson akizungumza katika eneo la tukio amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi ili kupata majibu sahihi ya tukio hilo na kutafuta suluhisho la matukio kama hayo yanayotokea mara kwa mara katika manispaa hiyo.

“Vyombo vya ulinzi vinaendelea kufatilia, sasa hivi inaonekana kata ya Kibeta katika hali ya ulinzi na usalama haijakaa sawa sawa kwahiyo mimi niombe vyombo vya ulinzi na usalama viweze kuongeza kasi katika suala la kufatilia na kujua nini kinachoendelea katika manispaa yetu ya Bukoba,” alisema Meya.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bukoba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, Erasto Sima amesema haijajulikana mauaji hayo yametokea saa ngapi lakini mwili wa mwanamke huyo umeokotwa alfajiri mbele ya nyumba ya Mwenyekiti na tayari polisi wameanza uchunguzi juu ya tukio hilo.

Rodri baba lao UEFA 2022/23
Haya hapa maagizo ya Kocha Nasreddine Nabi