Mwanamke mmoja, Olaide Adekunle (33), anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini Nigeria akidaiwa kumuuza mtoto wake Moridiat Rasaq (miezi 18), Naira 600,000 kwa mtu ambaye bado hajafahamika ili kulipa mkopo aliokuwa akidaiwa benki.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Msemaji wa Kamanda wa Polisi wa Jimbo la Ogun, SP Abimbola Oyeyemi amesema mshukiwa alikamatwa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa katika makao makuu ya tarafa ya Sango na mumewe, Nureni Rasaq.
Amesema, mume wa mshukiwa huyo aliripoti kuwa mkewe Olaide Adekunle, aliondoka nyumbani kuelekea Lagos Machi 15, 2023 akiwa na mtoto wao huyo wa kike, na alirudi nyumbani bila mtoto na kushindwa kutoa maelezo ya msingi.
Olaide Adekunle, anayeshikiliwa na Polisi kwa kuuza mtoto wake. Picha ya Within Nigeria.
SP. Oyeyemi amesema kitengo cha DPO Sango, kikiongozwa na CSP Dahiru Saleh, kilipeleka wapelelezi wake kumfuata mwanamke huyo, na alipokamatwa aliihojiwa na kukikiri kumuuza mtoto wake jijini huko Lagos kwa bei ya naira laki sita.
Amesema, alilazimika kufanya hivyo kwani alikopa pesa kutoka kwa benki ndogo ya fedha, na aliposhindwa kurejesha fedha hizo, mawakala wa benki walianza kumsumbua na kutishia kumshughulikia na ndipo alikimbilia Lagos na kufanikisha azma hiyo.
Kaimu Kamishna wa Polisi, DCP Babakura Muhammed, ameagiza mtuhumiwa huyo ahamishiwe Idara za Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa uchunguzi zaidi na kuangalia uwezekano wa kumpata mtoto huyo.