Mama mzazi wa Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans, Stephane Aziz Ki, Ki Sanata, amefichua kuwa mwanawe huyo huduma yake ilihitajika na Simba SC msimu liopita, lakini alikataa kutokana na aina ya uchezaji wa timu hiyo kuwa hauendani naye.

Akihojiwa na chaneli ya klabu hiyo, Bi. Ki Sanata, amesema Aziz Ki aliiona Simba SC ikicheza katika mechi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Februari na Machi 2022, alipokuwa akiitumikia ASEC Mimosas na kucheza mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Pia mama huyo ameweka hadharani kuwa mchezaji huyo alihitajika na timu mbili za Tanzania, moja ya Misri na nyingine Morocco, lakini mwisho wa siku akaamua kwenda kuichezea Young Africans.

“Alipokuwa ASEC Mimosas, klabu nne zilikuwa zinamtaka, Misri, Morocco na klabu mbili za Tanzania, aliwahi kucheza dhidi ya Simba hapa, lakini hakupenda aina yao ya uchezaji na akaanza kuangalia aina ya uchezaji wa Young Africans akaipenda, akaona aina yao inaendana na uchezaji wake,” amesema Bi. Ki Sanata.

Maelezo haya yanamaliza uvumi, tetesi au malumbano kama Simba SC ilikuwa inamtaka mchezaji huyo au la.

Wakati akisajiliwa na Young Africans, ilidaiwa kuwa Simba SC ilikuwa ya kwanza kumtaka, na hata baada ya kusajiliwa, baadhi ya viongozi wa timu hiyo walikataa katakata kuwa hawajawahi kutuma ofa au kumtaka mchezaji huyo.

Mama Aziz Ki amesema kijana wake hakufuata pesa Tanzania kwani alikuwa na ofa nyingine kubwa, lakini kwa sababu ameshacheza klabu mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika alichofuata ni kucheza kwa uhuru na amani kwani kuna matatizo mengi katika baadhi ya nchi ikiwamo upendeleo na ubaguzi.

“Mtoto aliniambia anataka kwenda kucheza akiwa huru na amani, kuna nchi zingine zina ubaguzi,” amesema.

Akieleza maisha ya kijana wake, alisema hakumaliza shule kwa sababu ya mpira wa miguu ambao alianza kucheza akiwa na miaka saba tu, huku mara kwa mara akiwa anatoroka au kutega shule.

“Naweza kusema alizaliwa ili acheze mpira, alianza kupenda soka ana miaka mitano tu, baba yake alikuwa anampenda mchezaji mmoja raia wa Morocco anaitwa Aziz Bouderbala na ndilo alilopewa yeye, alikuwa akiamka asubuhi kabla ya kunywa chai anakwenda kucheza uwanjani, baadae ndiyo anakwenda shule, watu wakaanza kutambua kipaji chake na ilikuwa ni kipindi ambacho anasoma, ila nikaja kugundua kuwa kuna wakati anakwenda shule, lakini wakati mwingine anatega, anatoroka kwenda kucheza mpira,” amesema.

Amesema mwaka wa pili akiwa shule ya sekondari alikataa kuendelea na masomo kwani soka lilikuwa kwenye damu.

“Mwaka wa pili akiwa sekondari akaniambia kuwa hataki shule, anataka kuendelea kucheza soka, nikamwambia hivyo vitu vyote vinatakiwa kwenda sambamba, Utasaini vipi mikataba wakati huna elimu?

Kwa sababu alisimamia msimamo wake, nikamuacha afanye anavyotaka kwa sababu aliniambia ana maono makubwa kuhusu soka, alipofikisha miaka 17 alikwenda Hispania na Ufaransa kwa ajili ya kucheza soka na kurejea baadae kwenye kikosi cha ASEC Mimosas,” amesema.

Mavunde kuendeleza mageuzi Sekta ya Madini
Bayern Munich kuinufaisha The Three Lions