Shughuli za kutafuta na kuopoa miili ya mama na mwanaye waliozama Septemba 29, mwaka huu katika feri ya Likoni nchini Kenya, zinaendelea kwa vikosi vya Serikali, sekta binafsi na vikosi kutoka Afrika kusini kushirikiana.
Vikosi vya wazamiaji kutoka Afrika kusini vimeongeza nguvu, lakini changamoto iliyobaki ni vifaa visivyo na ubora pamoja na kina kirefu cha bahari.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa huduma katika feri hiyo amesema timu ya wazamiaji kwa sasa itategemea zaidi teknolojia kusaidia kutambua vitu chini ya bahari na kupata mwili wa Mariam Kighanda (35) na mwanaye (4).
Mariam na mwanaye walifariki baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye kivuko kilipokuwa kinakaribia kutia nanga na kuzama baharini wakati wakivuka bahari kwa kutumia kivuko cha MV Harambee.
John Wambua ambaye ni mume na baba wa marehemu hao amesema kuwa uchungu wa kutokujua kama lini watapata miili ya wapendwa wao bado uneendelea kuitafuna familia hiyo.
” Miaka 13 niliyoishi na mkewangu ilikuwa bora sana, nasikitika sikuweza kuwa pale waliponihitaji zaidi kuwaokoa” amesema Wambua.
Ameongeza kuwa jambo pekee wanalohitaji kwa sasa ni kupata miili ya wapendwa wao na kuipumzisha wenyewe ili roho zao zipumzike kwa amani.