Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza wajumbe wa Tanzania kwenda nchini Burundi kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais, Evariste Ndayishimiye hapo kesho June 18,2020.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi Jijini Dar es Salaam katika Ubalozi wa Burundi Nchini Tanzania alipokwenda Ubalozini hapo kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aliyefariki June 09,2020 kwa maradhi ya Moyo.
Ameongeza kuwa kutokana na mahusiano ya karibu yaliyopo baina ya Burundi na Tanzania Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameamua kuongeza ujumbe wa Tanzania kwenda Burundi ambapo mbali na kuongozwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan pia ataambatana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete.
Prof. Kabudi amesema kuwa Hayati Pierre Nkurunziza amefanya kazi kubwa sana ya kuiunganisha Burundi na kuifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi zenye umoja na amani katika bara la Afrika lakini pia kuirejeshea Burundi matumaini na amani ya demokrasia na kudhihirika katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu na kumalizika kwa amani.
Kwa upande wake Balozi wa Burundi Nchini Tanzania Balozi Gervais Abayeho amesema Ubalozi huo na Warundi kwa ujumla wamepokea kwa mshtuko na majozi taarifa za kifo cha Rais Pierre Nkurunziza hasa ukichukulia kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi Rais huyo alikuwa akiendelea na shughuli zake kama kawaida ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi.
Rais Pierre Nkurunziza alifariki dunia June 09,2020 kutokana na ugonjwa wa moyo alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Natwe Turashoboye iliyopo mkoani Karuzi,mashariki mwa Burundi.