Binti mwenye umri wa miaka 16 (jina limehifadhiwa) mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kashenge iliyoko katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera, amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera akiuguza majeraha anayodai kuyapata baada ya kuunguzwa kwa maji ya moto na mama yake wa kambo.
Akizungumza kwa shida katika wodi namba kumi iliyoko katika hospitali hiyo, binti huyo amesema kuwa mama huyo wa kambo alifika nyumbani na kumkuta amepika viazi akamuuliza kwa nini alipika viazi bila kuambiwa, ndipo akammwagia chakula hicho pamoja na maji ya moto.
“Baada ya kuingia jikoni akakuta nimepika viazi alichukua sufuria na kunimwagia, niliamua kuondoka na kuingia ndani, akaja mdogo wangu akaniambia twende kwa mtendaji tukaenda hatujamkuta” amesema binti huyo.
Amesema kuwa mama yao mzazi alitengana na baba yao na kuwaacha wakiwa watano yeye na wadogo zake wanne.
Kwa upande wake afisa muuguzi msaidizi wa upande wa upasuaji, Edith Ezekiel amesema kuwa walimpokea binti huyo akiwa ameunguzwa mkono wa kulia na sehemu za bega na kuwa hali yake kwasasa sio mbaya na anaendelea na matibabu.
Aidha, Mama mzazi binti huyo aliyefahamika kwa jina la Alodia amesema kuwa akiwa nyumbani kwake wilayani Muleba alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa jirani na wanakoishi watoto hao, na kumwambia mtoto wake ameunguzwa kwa maji ya moto.
Naye kamanda wa polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema kuwa tukio hilo ambalo limeripotiwa polisi na kufunguliwa jalada la kujeruhi namba RB/2466/19, amesema hakuwa na taarifa ya tukio hilo na kuongeza kuwa atatoa taarifa rasmi Mei 24 mwaka huu.