Mwanaume mmoja aliyejaribu kuwaokoa wanawake watatu na mtoto mmoja waliokuwa wamekwama kwenye treni ya abiria iliyoanguka baada ya kugonga lori nchini Afrika Kusini amesema waliteketea kwa moto.

Tiaan Esterhuizen, aliyekuwa anakunywa chai karibu na eneo la tukio wakati treni hiyo ilipogongana na roli na kuanguka amesema kuwa alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika eneo hilo lakini juhudi zake hazikuzaa matunda aliyotarajia.

“Tuliona wanawake watatu wakiwa wamenasa kwenye treni, mmoja alikuwa analia sana na kutuelekeza kuwa kuna mtoto pia amenasa. Tulijaribu kumuangalia mtoto hatukufanikiwa, na naamini wote waliteketea kwa moto,” Esterhuizen aliliambia shirika la habari la AFP.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Mondi Mvambi aliiambia AFP kuwa waokoaji wanahofia kuwa miili zaidi itapatikana kadiri zoezi la kutafuta linavyoendelea.

Watu 14 wamepoteza maisha na wengine 268 wamejeruhiwa katika ajali hiyo. Baadhi ya watu wanadaiwa kuteketea kwa moto na miili yao kushindwa kupatikana na waliopatikana hawatambuliki.

Dereva wa lori lililogongana na treni hiyo ni mmoja kati ya majeruhi wanaopatiwa matibabu hospitalini.

Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.

Ndege yenye watu nane yaanguka
Jeshi lamuokoa msichana mikononi mwa Boko Haram