Beki wa klabu ya Young Africans Mamadou Doumbia amelazimika kuondoka nchini na kurejea nchini kwao Mali, kufuatia msiba wa Baba yake mzazi uliotokea jana Alhamis (April 13).
Doumbia aliyesajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu huu 2022/23 akitokea Stade Malien, ameondoka Dar es salaam mapema leo Ijumaa (April 14) kurejea nyumbani kwao Mali, kwa ajili ya kushiriki taratibu za Mazishi.
Klabu ya Young Africans imethibisha kuondoka kwa Beki huyo kupitia taarifa malum iliyosambazwa katika vyanzo vya habari vya klabu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara kwa sasa.
Taarifa hiyo imeeleza: Klabu ya Yanga imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Baba mzazi wa mchezaji wetu Mamadou Doumbia, kilichotokea jana, nchini Mali.
Mamadou Doumbia anataraja kusafiri asubuhi leo kuelekea Mali kwa ajili ya kushiriki taratibu za mazishi.
Kwa niaba ya Wanachama, Wapenzi na Mashabiki wa Yanga, Uongozi wa Klabu ya Yanga unatoa pole kwa mchezaji wetu Mamadou Doumbia na familia yake yote kwa msiba huu na Mwenyezi Mungu awatie nguvu kwenye kipindi hiki kigumu. Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi. Amina.