Kichaa cha Mbwa ni ugonjwa ulioathiri maeneo mbalimbali ya nchi yetu na maeneo mengine duniani, hususan bara la Asia na Afrika, unasababishwa na virusi jamii ya ‘lyssa’ ambavyo hukaa katika mate ya wanyama jamii ya mbwa walioathirika (mbwa, paka, mbweha, fisi na wengineo).

Virusi hawa hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo.

Yapo mambo muhimu ya kufanya ili kujikinga na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni pamoja na:

1. Endapo mtu ataumwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni. Kidonda kisifungwe. Kisha apelekwe haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa.

2. Mtu aliyeumwa na mbwa awahi kwenda kituo cha kutolea huduma za afya na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo, na ni muhimu kumaliza dozi.

Wizara imekwisha kutoa maagizo kwa mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa chanjo hizi zinakuwepo katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya wananchi watakaohitaji.

3. Wanyama jamii ya mbwa, paka wasiruhusiwe kulamba vidonda vya binadamu, kwani mate yao huweza kuleta maambukizi endapo wameathirika.

4. Wamiliki wa mbwa wahakikishe wanachanja mbwa wao dhidi ya kichaa cha mbwa mara moja kila mwaka na kupata cheti.

5. Mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana na mnyama aliyeambukizwa

6. Kuhakikisha mazingira yote ni safi, ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunamoishi.

7. Watoto wapewe elimu na wakatazwe kuchokoza mbwa wasiowajua njiani (kuvuta mkia/masikio, kumpanda mgongoni n.k.).

Faiza afunguka kwa mara ya kwanza kulizwa na harusi ya Sugu
Yanga yakwaa kisiki klabu bingwa Afrika