Abel Paul, Jeshi la Polisi – Dar es salaam.
Jeshi la Polisi kupitia Shule ya Udereva Kilwa Road VTC Academy Driving School na Shirika la Bima Zanzibar wameonyesha kwa vitendo namna ya kushirikiana katika kuboresha miundombinu na vifaa ambapo wametoa injini ya gari ambalo wanafunzi wanalitumia wakati wa mafunzo ya udereva chuoni hapo.
Akipokea injini hiyo kutoka kwa shirika la bima Zanzibar Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Lazaro Mambosasa amesema Jeshi hilo linathamini sana mashirikiano na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha linabaini, kuzuia na kutanzua uhalifu hapa nchini.
Amesema, kitendo cha kununua injini mpya ya gari lililokuwa likitumika na shule ya udereva itasaidia sana katika ufundishaji wa madereva na kuzalisha madereva bora wenye weledi ili kupunguza ajali hapa nchini huku akiwaomba walimu wa shule hiyo ya udereva kutunza vifaa hivyo vilivyotolewa na Zanzibar insurance.
Dkt. Mambosasa amebainisha kuwa, Jeshi hilo kupita kamisheni yake Polisi jamii imekuwa na utaratibu wa kushirikisha jamii katika maeneo tofauti tofauti kama ambavyo kamisheni hiyo chini ya kamishna wa Polisi Jamii CP Faustine Shilogile anavyotoa dira ya namna bora ya kushirikisha jamii katika kukabiliana na uhalifu hapa nchini.
Kwa upande wake meneja wa idara ya masoko wa shirika la bima Zanzibar, Bi. Amina Mohamed amesema wataendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika maeneo tofauti tofauti huku akiwaomba Jeshi hilo kuendelea kuzifurahia huduma bora za shirika hilo la bima Zanzibar na wananchi wengine.