Zikiwa zimesalia siku mbili, wakristo kuadhimisha sikukuu ya pasaka, Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam, limepiga marufuku mikusanyiko katika fukwe za bahari pamoja na kumbi za starehe kama bar ili kukinga maambukizi dhidi ya virusi vya Corona.
Akizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo April 9, 2020 Jijini Dar es salam, Kamanda wa polisi kanda maalum, Lazaro Mambosasa amesema lengo lao ni kuhakikisha wananchi wanaepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
” Katika kipindi chote cha pasaka, polisi kanda maalum imejipanga kuhakikisha hakuna uhalifu, vurugu na mikusanyiko isiyo ya lazima inafanyika ikiwa ni maelekezo ya serikali ya kujikinga na maambukizi ya corona” Amesema Kamanda Mambosasa.
Mapema leo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewaambia viongozi wa dini zote nchini kuwa Tanzania imefikia hatua ya kuwa na maambukizi ya ndani yaani visa vya hivi karibuni vyote wagonjwa wameambukizwa wakiwa ndani ya nchi hivyo jitihada zaidi zinahitajika kukabiliana na ugonjwa huo.