Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, IGP Simon Sirro amefanya mabadiliko kwa  baadhi ya makamanda wa jeshi hilo wa mikoa na kanda maalumu kwaajili ya kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kazi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es salaam na Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa imesema kuwa, aliyekuwa Kamishana Msaidizi Mwandamizi (SACP) Kamanda wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa ameteuliwa kuwa Kamishna Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, huku aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kamanda Lucas Mkondya akihamishiwa mkoani Mtwara.

Wengine waliofanyiwa mabadiliko ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, SACP Neema Mwanga ambaye amerudishwa makao makuu Dar es salaam ambapo atapangiwa kazi nyingine,

Aidha, sambamba na mabadiliko hayo taarifa hiyo imeeleza kuwa IGP Sirro amemteua DCP Juma Yusuph Ally kuwa Kaimu Kamishna wa Zanzibar huku ikieleza kuwa uteuzi huo umetokana na kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa aliyekuwa Kamishna wa Zanzibar, Hamdani Omari Makame.

Hata hivyo, taarifa hiyo imeongeza kuwa IGP Sirro amemteua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, SACP Gilles Mloto kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emmanuel Lukula kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke.

 

Meya: Madiwani wa Chadema waliojiuzulu wanaomba kurudi
UN yatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano Syria