Mlinda mlango wa kikosi cha Uganda kilichoshiriki fainali za Afrika za mwaka 2017 nchini Gabon Denis Onyango, amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu bingwa Afrika kusini na mabingwa wa Afrika, Mamelodi Sundowns.
Onyango amekubali kusaini mkataba wa miaka minne ambao utaendelea kumuweka nchini Afrika kusini hadi mwaka 2021.
Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 29, alicheza michezo miwili ya kwanza ya hatua ya makundi ya michuano ya AFCON, na alilazimika kukosa mchezo wa mwisho kufuatia majeraha yaliyokua yakimkabili.
Mwezi uliopita, Onyango alitangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani kwa mwaka 2016, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo mbalimbali iliyokua imeandaliwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF.
Onyango anakua mlinda mlango pekee na mchezaji wa kwanza kutoka nchini Uganda kuwahi kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo barani Afrika.