Mameya na maafisa wengine kutoka zaidi ya miji 50 kote duniani, wanakutana jijini London Uingereza kuanzia Machi 14 – 16, 2023 katika mkutano wa kwanza wa ushirikiano wa miji yenye afya, ili kushughilikia magonjwa yasiyoambukiza – NCDs na kuzuia majeraha.
Kukutana kwao, kunatokana na ushirikiano ulioanzishwa 2017 kwa wajumbe wa mtandao wa kimataifa wa miji 70 kutekeleza miradi na kuchagiza sera imara za afya ya umma katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kudhibiti tumbaku, chakula, usalama barabarani, kuimarisha ufuatiliaji wa NCDs na kuzuia watu kutumia kiwango cha kupitiliza cha dawa.
Shirika la Afya Duniani – WHO, linasema magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, magonjwa sugu ya kupumua na majeraha yanayosababisha asilimia 80 ya vifo vyote ulimwenguni.
Hata hivyo, haya yanajiri wakati idadi kubwa ya watu duniani wakiishi katika mazingira ya mijini, na shirika hilo linasema viongozi wa miji hiyo wako katika nafasi ya kipekee ya kubadilisha mapambano dhidi ya NCDs na majeruhi ikiwemo kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kutekeleza sera zilizothibitishwa.