Mamia ya waumini wa kanisa la Coptic nchini Misri jana walifanya maandamano makubwa wakielekea kufanya mazishi ya pamoja ya watu saba wa kanisa hilo waliouawa Ijumaa kwa kupigwa risasi, wakielekea kufanya ibada.
Waombolezaji waliokuwa na hasira na majonzi waliotoka kuwaombea marehemu hao katika kanisa la Prince Tadros katika jijini la Minya, walibeba picha za marehemu hao zenye jumbe mbalimbali.
Kundi la kigaidi la Islamic State (IS) lilitangaza kuhusika na mauaji hayo, ikiwa ni tukio lingine jipya la mauaji kufanywa na magaidi hao nchini Misri dhidi ya wakristo wa kanisa la Coptic.
Uongozi wa kanisa hilo ambalo lina waumini wachache kulinganisha na idadi ya waumini wa dini ya Kiislam, mwaka jana liliilalamikia Serikali kwa kutochukua hatua madhubuti za kuwalinda dhidi ya mashambulizi hayo baada ya watu 28 kuuawa Mei, 2017.
Shambulio hilo la Ijumaa lililolenga mabasi mawili katika jiji la Minya lilisababisha pia majeruhi saba ikiwa ni pamoja na watoto, kwa mujibu wa AFP.